Monday, 21 July 2014

UFUGAJI WA SAMAKI UTAINUA UCHUMI WA NCHI YETU?

SEKTA ya uvuvi ni miongoni mwa sekta tegemeo katika ukuaji wa uchumi wa hapa nchini, kwani huliingizia taifa mapato na fedha za kigeni yatokanayo na kodi na ushuru mbalimbali.
Rasilimali ya uvuvi hutoa ajira, chakula na ni kivutio kikubwa cha utalii. Kwa mujibu wa taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa ya mwaka 2008, katika kipindi cha miaka minne iliyopita, yaani tangu mwaka 2005/2006 hadi 2008/2009; sekta ya uvuvi imeweza kuingiza shilingi bilioni 1,041 katika pato la taifa.
Huu ni mchango mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu. Tanzania ina ukubwa wa km 942,600, ambapo asilimia 6.55 ya eneo hilo limefunikwa na maji.
Maji yote haya yana utajiri mkubwa wa rasilimali, ikiwemo samaki na bidhaa nyingine za majini zinazohitaji kulindwa, kuhifadhiwa, kuimarisha usimamizi na kutumiwa kwa manufaa endelevu ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Hata hivyo, miongoni mwa jamii nyingi ufugaji wa viumbe wa majini haujafikia hatua ya ufanisi kama ilivyo kwenye sekta nyingine za ufugaji au kilimo.
Wataalamu wa ufugaji wa samaki (Aquaculture) wanaona kuwa shughuli hiyo inaleta matumaini ya kupatikana kwa chakula chenye virutubisho kwa ajili ya idadi ya watu wanaoongezeka kwa haraka.
Uzalishaji wa samaki unaweza ukawa ni njia muhimu ya kuongeza kipato kwa jamii maskini ya vijijini na chanzo kizuri cha protini, hususan yanapotokea majanga ya magonjwa kama mafua ya ndege au homa ya bonde la ufa ambayo yamekuwa yanazuia jamii kutumia nyama ya kuku au ng’ombe.
Ufugaji wa samaki ni sekta inayokua kwa haraka duniani ikiwa inatoa lishe kwa watu milioni 250. Mwaka 1980, ni asilimia tisa tu ya samaki walipatikana kutoka kwenye maeneo wanamofugwa. Hivi sasa kiwango cha samaki wanaopatikana kiwango chake kimeongezeka na kufikia asilimia 44.
Mavuno ya samaki nchini yamefikia tani 350,000, kiasi ambacho ni kidogo kuliko uwezo wa wanaoweza kuvuliwa ambao ni tani 750,000. Samaki wengi wanaovuliwa nchini hutumika kama chakula, ukiacha samaki aina ya sangara, kamba na dagaa ambao huuzwa nje ya nchi.
Kwa kutegemea makisio ya ulaji samaki kwa mwaka ambao ni kilogramu 15 kwa kila mtu, inakadiriwa kuwa kiasi cha tani 368,878 zingehitajika mwaka 1990, japokuwa shughuli za uvuvi ziliweza kuzalisha kiasi cha tani 359,000, kiasi ambacho kilikuwa pungufu kwa tani 9,873, kinachotarajiwa kitokane na ufugaji wa samaki.
Ufugaji wa samaki kwenye mabwawa ndiyo aina ya shughuli za ufugaji wa samaki unaofanyika kwa kiasi kikubwa hapa nchini kutegemeana na hali ya hewa, mahitaji muhimu yanayohitajika katika shughuli ya ufugaji wa samaki ni pamoja na rasilimali watu na mitaji, ingawa mabwawa yameendelea kuchimbwa na idadi kubwa kuongezeka kila mwaka.
Mabwawa ya kufugia samaki yana faida ya kuzuia mmomonyoko wa ardhi, kusambaa kwa moto, maji kwa kunywesha wanyama, umwagiliaji, kuogelea, kuwa hifadhi kwa baadhi ya viumbe pori na mahala pa burudani au pumziko.
Katika mafunzo elekezi ya ufugaji bora wa samaki yaliyofanyika katika Wilaya za Mahenge, Kilosa na Mvomero mkoani Morogoro wafugaji wengi wamesema shughuli za ufugaji wa samaki hukabiliwa na matatizo na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa teknolojia bora, upungufu wa vifaranga bora, miundombinu ya usafiri duni, utafiti usiokidhi mahitaji, ukosefu wa takwimu za uzalishaji na upungufu wa taarifa sahihi za utunzaji wa mabwawa ya samaki.
Jabir Nassor, mfugaji wa samaki katika Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro anasema mafunzo kwa vitendo yatawasaidia wafugaji kutambua uzalishaji wa vifaranga vya samaki aina ya kambale, utambuzi wa jinsia ya kiume na kike kwa samaki aina ya perege na kambale na urutubishaji wa mabwawa kwa kutumia mbolea ya samadi.
Anasema iwapo wafugaji watapatiwa mafunzo ya uzalishaji wa vifaranga vya kambale, wakulima wa samaki wataweza kujiongezea kipato kwa kujizalishia vifaranga vyao na watakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuinua hali yao ya maisha na kuboresha aina ya ufugaji na kuwa wa kibiashara.
Mtaalamu wa ufugaji samaki kutoka nchini Marekani Edwin Requitina aliyetembelea mikoa ya ukanda wa pwani hapa nchini anasema ufugaji samaki ni mkakati mzuri wa kupambana na umaskini kwa wakazi wa pwani, mbali na kuboresha lishe kwa wananchi.
Anasema kukiwa na ushirikiano mzuri kutoka kwa wananchi, ufugaji wa samaki unaweza kuwa shughuli endelevu kwa wakazi wa pwani na itatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa taifa.
“Tumehamasika sana na matokeo ya ufugaji wa samaki, hususan katika Kijiji cha Changwaela, Bagamoyo, ambako mfugaji mmoja tayari amevua zaidi ya tani moja zilizompatia kipato kizuri. Sasa tunaweza kueneza ufagaji wa samaki katika wilaya nyingine za pwani bila wasiwasi wowote,” anasema Requitina.
Msimamizi wa mradi wa Taasisi ya Chama cha Wanasayansi katika Kanda ya Magharibi mwa Bahari ya Hindi (WIOMSA), Dk. Avit Mmochi, anasema mafanikio yanayopatikana yanaleta faraja na yanapaswa kuimarishwa zaidi.
“Juhudi zilizopo sasa zinapaswa kupongezwa na kadiri tunavyoelekeza taaluma na mikakati yetu katika kuboresha maisha ya wananchi, inatubidi tufanye mipango bora ya kutumia bahari na pwani yetu kwa manufaa endelevu. Ufugaji wa samaki utaongeza mapato ya wafugaji, licha ya kuboresha lishe katika kaya husika,” anasema Dk. Mmochi.
Anasema WIOMSA imejipanga kujifunza uzoefu kutoka katika nchi za Bara la Asia ambao wameendesha ufugaji samaki kwa zaidi ya miaka 100 sasa na kuhamisha ujuzi na uzoefu huo kwa mafanikio na faida nzuri nchini.
Naye Sandey Nundwe, ambaye ni mtaalamu wa kuchimba mabwawa ya samaki katika taasisi hiyo, anasema bwawa dogo uchimbwa kwa kutumia mikono na vifaa kama jembe, sururu na chepe, lakini mabwawa makubwa inabidi kutumia mashine za kuchimbulia udongo.
Anafafanua kuwa bwawa la samaki linatakiwa kuwa na kina kirefu upande mmoja na kina kinapungua kuelekea upande mwingine wenye kina kifupi na kwenye kina kirefu huwekwa bomba lenye chekeche la nyavu za mbu kwa upande wa ndani ya bwawa kwa ajili ya kutolea maji. Na bomba hili huzibwa lisitoe maji ila pale inapohitajika kupunguza maji.
Nundwe anasema baada ya bwawa kukamilika kuchimbwa hujazwa maji hadi juu ili kuangalia kama yanatuama au kuna kingo zinavuja, baada ya hapo huwekwa chakula cha samaki ambacho ni mbolea ya samadi mchanganyiko yaani ya kuku na ng’ombe kwa kipimo cha sehemu tatu za ng’ombe kwa moja ya kuku.
Kwa mujibu wa Nundwe bwawa lenye ukubwa wa ekari moja, kilo 80 za mchanganyiko wa mbolea ya samadi huitajika kila siku na chakula hukaa kwa siku tatu ndipo samaki huweza kuingizwa katika bwawa hilo.
“Unaweza kuwalisha mabaki ya vyakula, pumba na mboga mboga. Lisha samaki wako kwa siku sita na siku ya saba usiwalishe, punguza maji robo na kujaza mengine. Bwawa lenye ukubwa wa ekari moja linaweza kuchukua samaki aina ya tilapia 2,800-3,000 watakaokuwa tayari kuvunwa baada ya siku 90 hadi 120,” anasema Nundwe.
Mmoja wa wafugaji wa samaki kutoka Tabora wilayani Sikonge, Hassan Kisonta, anasema alijitosa katika shughuli hiyo miaka mitano iliyopita na sasa anamiliki mabwawa 15 ya samaki.
Anasema aliamua kuachana na kilimo cha tumbaku na kutafuta shughuli mbadala ya kufanya na kwamba anajutia miaka aliyoipoteza kwa kujishughulisha na kilimo cha tumbaku, kwani ni kigumu kutokana kusota shambani miezi karibu tisa na kinachopatikana hulipwa kwa mavuno ambayo ni kidogo mno.
“Maisha yangu sasa ni mazuri kuliko yalivyokuwa miaka iliyopita. Nimeweza kujenga nyumba ya kisasa ya vyumba sita kutokana na uuzaji wa samaki na kuwaacha wenzangu wanaolima tumbaku wakiendelea kuishi katika vijumba vyao vya udongo,” anasema Kasonta.
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, anasema serikali imeendelea kuhimiza ukuzaji wa viumbe hai kwenye maji kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa samaki na mazao mengine ya majini ili kuinua pato la taifa.
Kwa sasa kuna mabwawa 14,746 ya samaki aina ya perege na mabwawa 63 ya samaki aina ya ‘mwatiko’ na visima tisa vya samaki aina ya ‘trout’ ambapo uzalishaji unakadiriwa kuwa ni wastani wa tani 2.7 za perege kwa hekta.
Anasema katika jitihada za kuboresha sekta ya uvuvi, serikali kupitia ufadhili wa Benki ya Dunia ilianza kutekeleza Mradi wa Usimamizi wa Mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani (MACEMP) unaowezesha wananchi kuibua miradi ya ujasiriamali, ambapo hadi sasa miradi 124 yenye thamani ya sh bilioni 1.3 imeibuliwa.
“Kwa ujumla mradi huu unafadhili miradi tofauti, ikiwemo ya kilimo cha mwani, ujenzi wa maboti, ujenzi wa ngazi zinazoelekea baharini na kusokota kamba za usumba. Shughuli nyingine ni miradi ya utalii, ufugaji wa samaki na shughuli nzima za usimamizi na uhifadhi wa mazingira ya bahari,” anasema Wanyancha.
Kwa mujibu wa Waziri Wanyancha, kupitia maeneo tengefu ya bahari, serikali imetekeleza mpango wa kubadilishana zana haribifu kwa zana bora za uvuvi endelevu katika maeneo tengefu.
Hadi sasa wanajamii 275 kutoka Hifadhi ya Bahari ya Kisiwa cha Mafia na 217 kutoka Hifadhi ya Bahari ya Ghuba ya Mnazi na mwingilio wa Mto Ruvuma wamenufaika na utaratibu huo.
Anasema katika ukanda wa mwambao wa Bahari ya Hindi wawekezaji wamehamasishwa kujenga viwanda vya uchakataji wa mazao ya uvuvi na kuuza katika soko la ndani na nje.
Viwanda vitatu vinavyouza mazao ya uvuvi soko la ndani na nje kwenye Jumuiya ya Ulaya ni Bahari Food Ltd cha Dar es Salaam, Tanpesca kilichopo Mafia na Sea Product kilichopo Tanga.
Dk. Wanyancha anasema kuna viwanda vingine vitatu vinavyouza mazao ya uvuvi soko la ndani na nje. Viwanda hivyo ni Asmara Trading Company, Shamez Enterprises na Fruit de ler Mer vilivyopo Dar es Salaam.
Vilevile kuna viwanda viwili vipo katika hatua za mwisho za ujenzi, navyo ni Alpha Krust Ltd na Royal Africa Lobster Tropical vyote vya Dar es Salaam.
Maliasili ya uvuvi humalizika, hivyo lazima ilindwe, isimamiwe na kuendelezwa kwa misingi endelevu. Sera ya uvuvi haina budi kulenga katika kuondoa matatizo yanayoikabili sekta na kuainisha hatua zitakazochukuliwa.0 comments:

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Powered by Teknotaarifa