Friday, 5 September 2014

HADITHI YA MVUVI MASIKINI SEHEMU YA KWANZA

Hadithi, Hadithi. Hapo zamani za kale aliishi mvuvi masikini ambaye kwa jina aliitwa Majuto. Majuto aliishi kwenye kijiji kidogo pembeni mwa ziwa dogo pamoja na familia yake. Kwa miaka mingi sana watu wa kijiji hicho walikuwa wakiishi wakitegemea ziwa hilo kwaajili ya samaki na maji kwa matumizi yao yote. Waliweza kukamata samaki wakuwatosha wao na pia wachache ambao waliweza kuuza kwenye vijiji vya jirani ili kujipatia mahitaji mengine. Kila asubuhi Majuto aliamka mapema na kutayarisha ngalawa na ndoano yake na kwenda kuvua samaki ili aweze kuipatia familia yake chakula. Ngalawa yake ilikuwa ni kubwa na imara sana yenye uwezo wa kwenda umbali mrefu juu ya maji bila tatizo lolote. Lakini Majuto alikuwa sio mvuvi mzuri kwa kuwa aliogopa sana maji na hakujua kuogelea. Kila siku aliwaza sana kabla ya kupanda ngalawa yake na alifikiria itakuwaje kama ikizama au ikipata shida ya aina yeyote na akadumbukia kwenye maji. Ni kwa sababu tu alikuwa hana njia nyingine ya kujipatia yeye na familia yake chakula ndio alilazimika kwenda na kuvua samaki. Rafiki zake Majuto walijaribu kumfundisha jinsi ya kuogelea lakini kila alivyoweka tu mguu wa kwanza ndani ya maji alihisi kama vile anazama na aliamua kukimbia. Kweli tatizo lake la kuogopa maji lilikuwa ni kubwa na ni sugu. Kila asubuhui Majuto alienda na ngalawa yake kuvua samaki lakini aliishia tu kutega ndoano yake kandokando mwa ziwa ambapo hapakuwepo na samaki wengi. Alifanikiwa kumkamata samaki mmoja mmoja tu na ndoano yake na mwisho wa siku alikuwa amekata jumla ya samaki watatu au wanne tu wadogo. Hili jambo liliendelea kila siku, aliondoka asubuhi na mapema na alirudi jioni na samaki wachache sana. Uwoga wake wa maji ulimsababisha asiweze kufanikiwa zaidi kama walivyo fanya wavuvi wengine ambao waliweza kwenda umbali mrefu zaidi na kukamata samaki wengi zaidi waliokuwa wakubwa. Masikini Majuto siku zilivyopita uwonga wake haukupungua na alibakia kuwaza sana jinsi atakavyofanya ili aweze kupata samaki wengi zaidi. “Jamani jamani, nitafanya nini masikini mimi. Mbona wenzangu wanafanikiwa na mimi nashindwa 

JE SIKU ILIYOFUATA MAJUTOA ALICHUKUA HATUA GANI ILI KUFANIKISHA LENGO LAKE NAYEYE AWE NA SAMAKI WENGI KAMA WENGINE, USIKOSEA KUSOMA HADITHI PEKEE NA TAMU KATIKA BLOG HII.

0 comments:

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Powered by Teknotaarifa