Thursday, 30 April 2015

UHIFADHI BORA WA CHAKULA CHA SAMAKI

UHIFADHI WA UBORA WA MALIGHAFI NA CHAKULA CHA SAMAKI
1.0 UTANGULIZI
Chakula cha samaki ni moja ya mahitaji muhimu yanayotumia gharama kubwa katika ufugaji wa samaki. Kwa hiyo udhibiti mzuri wa ubora wa chakula unaweza kupunguza sana gharama zisizo za lazima na kumhakikishia mfugaji kuwa atapata samaki wenye afya nzuri na wengi na hivyo kuongeza uzalishaji. Kwa hiyo usimamizi mzuri na udhibiti wa ubora wa chakula cha samaki ni muhimu sana. Usimamizi na udhibiti wa ubora wa chakula huhusisha mambo muhimu yafuatayo: ufuatiliaji wa karibu wa ubora wa malighafi za kutengenezea chakula (feed ingredients) wakati wa utunzaji, utengenezaji, uchanganyaji na wakati wa kuhifadhi chakula baada ya kutengenezwa.

2.0 UTARATIBU WA UDHIBITI WA UBORA WA CHAKULA CHA SAMAKI
2.1 MAHITAJI
Ni muhimu kuhifadhi malighafi ya kutengenezea chakula cha samaki ili kuweza kudhibiti ubora wake. Hii husaidia kuhakikisha kwamba chakula kitakachotengenezwa kitakuwa na viwango/ubora utakaosababisha samaki watakaokila wawe na afya nzuri na wakue haraka. Mahitaji kama vile mahindi, ngano, dagaa n.k yanapokuwa yamehifadhiwa vizuri huepusha utengenezaji wa vyakula vilivyo na viwango/ubora hafifu.Vyakula bora huepusha samaki kupatwa na madhara ya kifya kama vile magonjwa na ukuaji duni. Viwango sahihi ni vile ambavyo vimefanyiwa utafiti na kukubalika kwamba vinafaa. Ni muhimu sana mfugaji/mtengenezaji wa vyakula ahakikishe kuwa anafuatilia na kutekeleza ushuri wa viwango uliopitishwa na watafiti/ wataalamu wa viwango ili kupata mafanikio makubwa katika shughuli ya ufugaji wa samaki. 

2.1.1 UKAGUZI WA VYAKULA
Ili kufanikiwa zoezi la udhibiti wa ubora wa chakula ni muhimu kufanya ukaguzi wa malighafi pamoja na chakula cha samaki kabla ya kuhifadhi, wakati wa kutengeneza chakula na hata wakati wa utunzaji vyakula.
Ukaguzi huu unahusu:
a.       Kuhakikisha kuwa vimekauka vizuri.
b.      Kuondoa takataka zote mfano mawe, vyuma, nyasi na uchafu mwingine wowote.
c.       Kuondoa wadudu wa aina zote
Vyakula vikiwa havijakauka vizuri/ vikiwa na unyevunyevu  ni rahisi kuoza,
kuota ukungu na hiyo kupunguza au kuharibu ubora ya chakula.
Mfano mahindi, mashudu ya karanga yanapohifadhiwa yakiwa hayajakauka au
kuhifadhiwa sehemu yenye unyevunyevu huweza kutengeneza sumu (aflatoxin)
itokanayo na ukungu huweza kuleta madhara kwa samaki. Kwa hiyo vyakula
vyenye unyevunyevu viendelee kuanikwa hadi vikauke ndipo vihifadhiwe.
Baadhi ya virutubisho vingine vilivyoko kwenye chakula kuharibika kwa urahisi endapo vyakula havitatunzwa vizuri. Mfano vyakula vyenye asili ya protein na mafuta huaribika kama vitawekwa kwenye mazingira ya joto kali au sehemu zenye unyevunyevu.

2.2 VYAKULA VILIVYOTENGENEZWA (processed food)

Udhibiti wa ubora wa vyakula hivi huusisha ukaguzi wakati wa matengenezo (processing) ya chakula ili kuhakikisha kuwa mahitaji yote muhimu yamechanganywa kwenye chakula kwa vipimo sahihi na katika hali ya usafi.  Ni muhimu kukagua chakula kama  mchanganyiko wa malighafi zilizomo ndani ya hicho chakula,  ni ule ulioshauriwa na wataalamu na kama chakula ni kikavu, hakijaoza, hakina ukungu au kukaa muda mrefu mno tangu kitengenezwe .
3.0 MADHARA YA KUTOKUZINGATIA UBORA WA VYAKULA
Vyakula vyenye unyevunyevu ni rahisi kuoza na kuota ukungu. Hali ya ukungu na kuoza hupunguza au kuharibu bora wa chakula. Hali hii inapotokea kwenye vyakula vilivyohifadhiwa vibaya huweza kutengeneza sumu mfano sumu ya aflatoxin ambayo hupatikana kwenye vyakula kama vile mahindi na mashudu ya karanga yaliyoota ukungu. Pia baadhi ya viini lishe huweza kuharibika na kupoteza ubora wake visipotunzwa vizuri na kukaguliwa mara kwa mara. Mfano vyakula vyenye asili ya protein na mafuta huaribika kama vitawekwa kwenye mazingira ya joto sana na unyevunyevu hata kusababisha upungufu wa ubora wakati wa utunzaji.
 HITIMISHO

Malighafi za kutengenezea chakula cha samaki pamoja na chakula kichokwisha tengenezwa huweza kubadilika wakati wa utunzaji. Mabadiliko haya yanapohusisha vyakula vya kutengenezea chakula husababisha hasara ya moja kwa moja kwa sababu husababisha upungufu wa ubora wa chakula. Mabadiliko kwenye vyakula vilivyokwisha tengenezwa hayahusishi tu upungufu wa thamani yake kilishe, bali pia huweza kuharibu hata ladha yake. Hali hii inaweza ikawapunguzia samaki hamu ya kukila hivyo kusababisha hasara. Kwa hiyo ili kudhiti upungufu wa ubora wa malighafi na vyakula vilivyotengenezwa tayari ni muhimu kuvihifadhi mahali pakavu,  pasipo na joto kali na pasafi kadiri iwezekanavyo.  Vyakula vitunzwe sehemu iliyoko juu visiwekwe sakafuni hata kamani pasafi.

0 comments:

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Powered by Teknotaarifa