Saturday, 4 July 2015

SOMA HADITHI HII UPATE KUFAHAMU SABABU ZA BAADHI YA WAVUVI WALIO WENGI NI MASIKINI.


Naanza kwa Hadithi, Hadithi.
Hapo zamani za kale aliishi mvuvi masikini ambaye kwa jina aliitwa Majuto. Majuto aliishi kwenye kijiji
kidogo pembeni mwa ziwa dogo pamoja na familia yake. Kwa miaka mingi sana watu wa kijiji hicho
walikuwa wakiishi wakitegemea ziwa hilo kwaajili ya samaki na maji kwa matumizi yao yote. Waliweza
kukamata samaki wakuwatosha wao na pia wachache ambao waliweza kuuza kwenye vijiji vya jirani ili
kujipatia mahitaji mengine.
Kila asubuhi Majuto aliamka mapema na kutayarisha ngalawa na ndoano yake na kwenda kuvua samaki
ili aweze kuipatia familia yake chakula. Ngalawa yake ilikuwa ni kubwa na imara sana yenye uwezo wa
kwenda umbali mrefu juu ya maji bila tatizo lolote. Lakini Majuto alikuwa sio mvuvi mzuri kwa kuwa
aliogopa sana maji na hakujua kuogelea. Kila siku aliwaza sana kabla ya kupanda ngalawa yake na
alifikiria itakuwaje kama ikizama au ikipata shida ya aina yeyote na akadumbukia kwenye maji. Ni kwa
sababu tu alikuwa hana njia nyingine ya kujipatia yeye na familia yake chakula ndio alilazimika kwenda
na kuvua samaki. Rafiki zake Majuto walijaribu kumfundisha jinsi ya kuogelea lakini kila alivyoweka tu
mguu wa kwanza ndani ya maji alihisi kama vile anazama na aliamua kukimbia. Kweli tatizo lake la
kuogopa maji lilikuwa ni kubwa na ni sugu.
Kila asubuhui Majuto alienda na ngalawa yake kuvua samaki lakini aliishia tu kutega ndoano yake
kandokando mwa ziwa ambapo hapakuwepo na samaki wengi. Alifanikiwa kumkamata samaki mmoja
mmoja tu na ndoano yake na mwisho wa siku alikuwa amekata jumla ya samaki watatu au wanne tu
wadogo. Hili jambo liliendelea kila siku, aliondoka asubuhi na mapema na alirudi jioni na samaki
wachache sana. Uwoga wake wa maji ulimsababisha asiweze kufanikiwa zaidi kama walivyo fanya
wavuvi wengine ambao waliweza kwenda umbali mrefu zaidi na kukamata samaki wengi zaidi
waliokuwa wakubwa.
Masikini Majuto siku zilivyopita uwonga wake haukupungua na alibakia kuwaza sana jinsi atakavyofanya
ili aweze kupata samaki wengi zaidi. “Jamani jamani, nitafanya nini masikini mimi. Mbona wenzangu
wanafanikiwa na mimi nashindwa”, alilalamika Majuto. Aliwaza sana mpaka ghalfa wazo lilimjia –
“nitaenda kumuomba mchawi anisaidie na kuniondolea shida zangu zote”, alisema Majuto. Pamoja na
kuwa alishasikia kwa wazee wa kijijini na pia kwa watu wengi kuwa mchawi huyo aliyekuwa akiishi
milimani sio mtu mzuri, Majuto hakufikiri mara mbili. “Hii ndio nafasi yangu kubwa ya kuweza
kubadilisha maisha yangu kabisa. Hao wanaosema kuwa hili sio jambo zuri hawapendi kuniona
nimefanikiwa”, alisema Majuto.
Hadithi Ya Mvuvi Masikini
Siku ikawadia na Majuto alifungasha virago vyake, aliiaga familia yake na kubeba zawadi ambazo alikuwa
amemtayarishia mchawi. Bila kugeuka aliondoka upesi na kuelekea juu milimani alipokuwa akiishi huyo
mchawi. Safari ilikuwa ni ndefu lakini Majuto alikuwa akitembea upesi sana. Alivuka mito, mabonde na
misitu minene ambamo walikuwa wakiishi wanyama wengi wakali. Baada ya kutembea kwa muda mrefu
Majuto alijikuta akipita kwenye uwanja mkubwa na kwa ghafla alitokea ndege mkubwa sana angani.
Alikuwa na rangi ya zambarau na njano na mkia mrefu wa kuvutia. Majuto alishtuka sana alivyomuona
huyo ndege kwa kuwa hakuwahi tena kuona ndege mkubwa hivyo aliyeruka angani. Alisimama mdomo
wake ukiwa wazi kwa mshangao. Ndege huyo alitua chini ardhini na alizidi kumsogelea Majuto. Jasho
jembamba lilimtoka Majuto na hakujua cha kufanya na alibaki amesimama tu bila kusema neno lolote.
Ndege alisimama na kumuangalia Majuto machoni kisha akasema kwa sauti nzito, “Mtaka vyote hukosa
vyote”. Kisha ndege aligeuka na kuruka angani na kupotea juu ya mawingu. Majuto hakuamini
alichokiona na kusikia na alijihisi anaota. Alijaribu kutafakari lakini alikosa jibu na akaamua aendelee na
safari yake ya kwenda kwa mchawi.
Baada ya kutembea kwa muda mrefu Majuto hatimaye alifika kwenye nyumba aliyoishi mchawi. Ilikuwa
ni nyumba kubwa nyeupe iliyovutia sana. Mawe meupe yaliyo ng’aa yalikuwa yamepangwa vizuri
kuelekea hadi mlangoni. Majuto alikuwa anauoga lakini alijikaza na akagonga mlango. ”Nani wewe?”,
alisikia sauti ikitoka ndani ya nyumba. ”Ni mimi Majuto mvuvi masikini. Nimekuja kuomba msaada
wako”. Mlango ulifunguliwa na hapo alikuwa amesimama mzee mmoja mfupi mwenye mvi nyingi.
Alionekana ni mtu wa kawaida tu tofauti kabisa na hadithi zote alizokuwa amezisikia Majuto huko kijijini
kwake. Majuto aliwaza kuwa labda amekosea nyumba na huyu sio yule mchawi ambaye watu walikuwa
wakimsema. Ikabidi Majuto amulize ”je, wewe ndio mchawi?”. ”Ha ha ha” alicheka mzee, ”ndivyo watu
wanapenda kuniita hivyo. Karibu sana ndani”.
Majtuo aliingia na kukaa chini kwenye mkeka. ”Ninaweza kukusaidiaje?” aliuliza mchawi. ”Nimefunga
safari kutoka mbali kuja huku ili niombe msaada wako”, alisema Majuto. ”Mimi ni mvuvi lakini
ninaogopa sana maji na hivyo inanizuiya kuweza kwenda mbali na ngalawa yangu ili nikatege ndoano
yangu na kukamata samaki. Kila ninavyowaza jinsi ya kufanya nashindwa na ninabakia tu kando kando
mwa ziwa ambapo samaki ni wachache na pia ni wadogo. Ninakuomba sana unisaidie kuondoa uwoga
wangu wa maji ili niweze kujifunza kuogelea na kupata uhodari wa kwenda mbali zaidi na ngalawa
yangu.” ”Lo, nimekuelewa”, alisema mchawi. ”Tatizo lako ni dogo sana. Subiri hapa nitakuletea dawa
itakayo kusaidia”. Mchawi aliamka na kwenda uwani. Baada ya muda si mrefu alirudi huku ameshika
chungu kidogo chenye kilichofanana na maziwa. Alimpa Majuto kile chungu na kumwambia anywe.
Hadithi Ya Mvuvi Masikini
Majuto alifanya hivyo. Baada tu ya kumaliza alisikia tumbo lake lina nguruma na mwili wote ulisisimka.
Alianza kujisikia wa tofauti kama vile amekuwa mwepesi zaidi. Mchawi akamwambia Majuto, ” Hii dawa
imekufanya uwe mwepesi na kuanzia leo utaweza kuogelea bila ya kuzama”. Majuto alifurahi sana na
kumshukuru mchawi kwa msaada wake. Kuonyesha shukurani yake Majuto aliitoa zawadi yake
aliyomletea na kumpa.
Wakati wa kuagana ulipofika Majuto alikuwa tayari kuondoka. ”Asante sana mzee, sasa mimi nitarudi
kjijini kuendelea na maisha yangu”, alisema Majuto. ”Ngoja kidogo.” Alisema mchawi. ”Kwani wewe
usingependa nikuwezeshe pia kukamata samaki wengi zaidi? Kwanini nisikupe kifaa ambacho
kitakuwezesha kukamata samaki wengi sana?” Majuto hakuamini alichosikia. “Mzee, yaani kuna kifaa
ambacho kitaniwezesha kukamata samaki wengi zaidi?”, alisema Majuto. “Ndio, nitakupa lakini itabidi
ukubaliane na masharti yangu kwanza”, alisema mchawi. “Niambie tu na mimi nitayatekeleza”, alisema
Majuto.
Mchawi aliondoka tena kuelekea uwani na kurudi na nyavu kubwa. Majuto hakuelewa ni nini kile
alichokuwa amekishika mchawi kwa kuwa hakuwahi kuona nyavu maishani mwake. Siku zote yeye na
wavuvi wenzake walikuwa wakitumia ndoano tu kuvulia samaki na hawakujua nyavu ni nini. Mchawi
akasema, “Hii ni nyavu. Iweke ndani ya maji kila jioni, utakapo rudi jioni utakuta samaki wengi sana
wamenasa kwenye matundu. Kazi yako itakuwa ni kuwaokota tu na kuwaweka ndani ya ngalawa yako.”
Majuto hakuamini masikio yake. ”Kweli hii ni siku ya furaha sana maishani mwangu. Lakini kwanini
unataka kunifanyia haya yote?” aliuliza Majuto. Mchawi alimjibu, ”Hapo zamani niliwakosea watu wengi
na nilifanya mambo mengi mabaya. Ndio maana ilinibidi nikimbilie na kuishi mwenyewe huku milimani.
Lakini nimefikiria sana mambo niliyoyafanya na nimeyajutia ndio maana ninataka kuwasaidia watu.
Sitakuomba mengi, lakini kila utakapoenda ziwani kuvua samaki ninataka uchukue nusu ya samaki wote
uliowashika na kuwapa masikini na wazee wasiojiweza. Ukishindwa kuyatekeleza haya basi na wewe pia
hautafanikiwa” Majuto haikumbidi hata kufikiria sana na alijibu, ”Mimi pia ninapenda sana kwasaidia
watu lakini tu sikuwa na uwezo. Sasa umeniwezesha na mimi pia nitawasaidia watu wengine zaidi ya
hata uliyoniambia.”
Kwa maneno hayo waliagana, na Majuto alibeba nyavu aliyopewa na mchawi na kuelekea tena kurudi
nyumbani. Alikuwa na furaha kubwa sana na alikimbia upesi sana hadi kufika nyumbani kwake.
Hakuwaza hata kusimama na kusalimia familia yake na kuwaambia kuwa amerudi, alikimbia moja kwa
moja hadi kwenye ziwa na kujitupa kwenye maji. Na kweli mchawi alivyokuwa amesema Majuto
hakuzama. Alibaki tu juu ya maji akielea. Majuto alishangilia sana na kwenda kuwatangazia rafiki zake


wote yaliyomkuta. Nao pia wakabaki kufurahi naye kwasababu Majuto alikuwa ni rafiki yao wa siku
nyingi.
Jioni ilivyofika na wavuvi wengine wakiwa wanarudi majumbani mwao, Majuto ndio alianza kuandaa
ngalawa yake. Alizipandisha nyavu alizopewa na mchawi huku akitabasamu. ”Leo ndio maisha yangu
yanabadilika, shida zangu zote ninaziacha nyumba”, alisema Majuto. Alipanda ndani ya ngalawa yake na
kuondoka kuelekea ziwani. Giza lilikuwa linaingia taratibu lakini Majuto hakuwa na wasiwasi kabisa na
alizidi kwenda mbali. Baada ya kusogea kwa muda, miti iliyokuwa ikiota kando mwa ziwa ilizidi
kuonekana midogo. Nyumba za kijiji nazo zilizidi kuonekana ndogo alivyozidi kwenda mbali. Alikuwa
amebakia mwenyewe tu kwenye ziwa, watu wote walikuwa wamesharudi majumbani kwao na
kupumzika kwa siku hiyo.
Ghafla Majuto alisikia mlio wa ndege ikitoka angani. Aligeuka kwa haraka na kuangalia juu. Ilikuwa ni
kama ndoto imejirudia, yule ndege mkubwa aliyejitokeza kwenye safari yake ya kwenda kwa mchawi
alikuwa amerudi. Majuto aliogopa sana kwa kuwa alijua yuko peke yake na hakuna mtu wa kumpa
msaada wowote. Ndege alizunguka ngalawa mara mbili halafu akatua juu ya yake. Walibaki
wanaangaliana tu kwa muda mrefu kisha ndege akafungua mdomo akasema, ”Mtaka vyote hukosa
vyote”. Kisha ndege aligeuka na kuruka angani na kupotea juu ya mawingu. Majuto alibaki tena kuwaza
sana nini maana ya hayo maneno. Kwanini ndege amwambie kuwa akitaka vyote atakosa vyote? ”Mimi
sina tamaa”. Alisema Majuto. ”Kwa hivyo ninajua kuwa sitaweza kupata shida ambazo ameniambia
ndege”.
Basi Majuto aliendelea hadi sehemu ambapo wavuvi wengine walisema kuwa kuna samaki wengi.
Alishusha nyavu ndani ya maji kama mchawi alivyokuwa amemwelekeza. Nyavu zilikuwa ni nyepesi na
alifanikiwa kuziweka ndani ya maji bila ya kupoteza muda. Alibaki kusubiri hapo hapo mpaka giza
likaingia bila ya kitu chochote kutokea. ”Mchawi aliniambia kuwa nitakamata samaki wengi sana lakini
Mbona hakuna dalili yeyote hapa?”, alisema Majuto. Masaa yalizidi kusogea na giza lilitanda lakini
Majuto alivumilia huku akisubiri ishara yoyote kuwa kuna samaki amekamatwa lakini hapakutokea kitu.
Usingizi ulianza kumshika Majuto na baada ya muda si mrefu alisinzia.
Mjuto hakuamka mpaka pale ambapo jua linaanza kuchomoza upande wa pili mwa ziwa. ”Kweli
nimehangaika bure”, alisema Majuto. ”Nimekesha usiku mzima na hakuna samaki hata mmoja.” Kwa
huzuni kubwa alianza kuzivuta nyavu iliazirudishe kwenye ngalawa. ”Mbona nyavu zimekuwa nzito
sana?”, alijiuliza. ”Au ni kwa kuwa zimeloa?”. Alizidi kuvuta kwa nguvu zake zote ndio nyavu zikaanza
Hadithi Ya Mvuvi Masikini
kupanda taratibu. Majuto aliangalia kwa makini zaidi na alishtuka kuona kuna samaki mmoja amekwama
kwenye nyavu. Alizidi kuvuta nyavu na mara akaonekana samaki mwengine mkubwa zaidi naye
amekwama kwenye nyavu. Majuto alizidi kufurahi na kuvuta nyavu kwa nguvu zaidi. Kila akizivuta na
samaki wengi wakubwa walikuwa wakizidi kupanda juu. Majuto alishangilia kwa sauti kubwa na kupiga
kelele kwa furaha. Alimalizia kupandisha nyavu na kuanza kuhesabu samaki. Walikuwa ni wakubwa na
wengi sana mpaka alishindwa kuhesabu wote. Majuto hakupoteza muda, aligeuza ngalawa yake na
kuelekea kurudi kijijini.
Majuto alipokaribia kufika aliiona familia yake na rafiki zake wengi wakimsubiri kando ya ziwa.
Aliwapungia mkono kuwaonyesha kuwa kila kitu kilikuwa ni salama. Kweli ilikuwa ni siku ya furaha
kubwa kwa Majuto na familia yake yote. Majuto aliwapa rafiki zake wote samaki. Pia aliwapa masikini na
wazee wasiojiweza kama mchawi alivyokuwa amemwelekeza Majuto. Watu wote siku hiyo walifurahi
kwa pamoja. Pamoja na kwamba alikuwa amewapatia ndugu na marafiki samaki wengi bado alikuwa
amebakiwa na wengine wengi. Majuto alipeleka samaki waliobaki sokoni na kuwauza kwa bei nzuri sana
na kupata fedha nyingi.
Maisha ya Majuto na familia yake yalibadilika. Kila jioni Majuto alienda ziwani na kutega nyavu zake na
kurudi asubuhi na samaki wengi sana. Nusu ya samaki wote aliokamata aliwapa masikini na wazee,
baada ya hapo alienda sokoni na kuuza samaki waliobaki kwa faida kubwa. Haikuchukua muda mrefu na
Majuto alipata uwezo wa kujenga nyumba kubwa ya kifahari yenye vyumba vingi. Nje alipanda bustani
kubwa ya maua na kufuga wanyama na ndege wengi wa kifahari kutoka nchi za mbali. Pia alikuwa na
wafanyakazi wengi wa ndani ambao walifanya kazi zote za ndani ili mke wake na watoto wake wasipate
taabu yeyote. Majuto alianza kujivuna na mali zake na hatimaye aliamua kuwa kazi ya kwenda ziwani
kila siku kukamata samaki haimfai yeye, aliamua kuajiri vijana wachache wakufanya hiyo kazi. Kweli
maisha yake na familia yake yalikuwa ni mazuri.
Usiku mmoja Majuto alikuwa amelala kitandani ndoto ikamjia. Aliota kuwa yuko kwenye chumba kidogo
kisichokuwa na madirisha wala milango. Alijaribu sana kutoka lakini alishindwa. Ghalfla yule ndege
mkubwa ambaye Majuto alishakutana naye mara mbili alitokea. Ndege alibaki tu anamwangalia Majuto
kisha akasema, “Mtaka vyote hukosa vyote.” Kisha ndege akapotea. Majuto aliamka kwa mshituko
mkubwa lakini alivyojua kuwa ni ndoto tu alitulia kidogo. “Lah, kumbe ni ndoto tu.” Alisema Majuto.
Alitafakari ndoto yake kwa muda mfupi lakini hakuona kama vile ni jambo lolote la kushitua na akarudi
kulala. Kesho yake maisha yaliendelea kama kawaida.


Lakini haikuwa ni rahisi kutunza vyote hivi mwenyewe na kisha ilimbidi Majuto kuajiri wafanyakazi wengi
wa kutunza nyumba na mali zake zote. Pia Majuto alianza kuwa na wasiwasi juu ya usalama wake.
Alifikiria kuwa kama haya yote yametokana na yeye kuwa na nyavu, je nyavu hii ikipotea au ikiibiwa,
itakuwaje? Basi aliamua kuajiri walinzi wengi pia wakumlinda yeye na mali zake zote. Walinzi wengine
aliwaajiri kwa kulinda nyavu tu.
Pamoja na mali zake zote Majuto alizojikusanyia, bado alikuwa anataka mengine mengi. Alitaka awe na
nyumba kubwa zaidi na ya kifahari zaidi. Alipenda awe na wanyama wengi wa kutoka nchi za mbali zaidi
na wafanyakazi wengi zaidi. Pia alitaka aweze kusafiri nchi za mbali na aweze kurudi na zawadi nyingi
kwa ajili ya familia yake.
Mali za majuto zilivyozidi kuwa nyingi na taabu na mawazo yalizidi kuwa mengi. Gharama za kulipa
wanfayakazi wake wote zilizidi na baadala ya kufurahia maisha yake mazuri alianza kuwaza sana. “Haya
yote nitaweza kuyatekeleza kweli iwapo nusu ya kipato changu chote nitaendelea kuwapa masikini?”
Alisema Majuto. “Hata hivyo nimeshawasaidia vya kutosha. Kuanzia sasa itabidi nianze kujifikiria
mwenyewe na matakwa yangu.” Kuanzia siku hiyo Majuto aliamua kuwapa masikini robo tu ya mapato
yake. Majuto alifikiria, “Mchawi kweli aliniambia niwape masikini nusu ya mapato yangu yote, lakini kwa
sasa ninadhani nimeshawasadia vya kutosha. Kwani mchawi atajuaje kuwa siwapi masikini nusu ya
mapato yangu.” Kufanya hivi kulimwezesha kuendeleza maisha yake ya kifahari. Alijenga nyumba kubwa
zaidi na kuajiri wafanyakazi wengi zaidi. Pia alisafiri mbali zaidi na kurudi na zawadi nyingi zaidi kwa
familia yake.
Lakini kama ilivyokuwa mara ya kwanza, gharama za kutunza mali zake zote zilizidi kuwa kubwa.
Hatimaye Majuto aliamua kuwapa masikini robo ya mapato yake haitawezekana tena. Aliamua kuwa
kuanzia sasa yeye mwenyewe ndio atakayefaidika na kazi yake. Aliacha kabisa kuwasaidia masikini na
wazee na pia tabia yake ilibadilika. Majuto hakuwa tena mtu mwenye roho nzuri kama watu
walivyokuwa wakimfahamu. Alibadilika na kuwa mtu mwenye hasira za haraka na alibaki kugombana
sana na watu, hata rafiki zake wa karibu. Mtu yeyote mwenye shida akimfuata Majuto alikataa kabisa
kumpa msaada hata kama alikuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Mara nyingine alitumia hata walinzi
wake kuwafukuza watu hao wenye shida.
Hadithi Ya Mvuvi Masikini
Siku moja Majuto alikuwa akitembea kwenye bustani yake alitokea bibi kizee mmoja na kumwambia
Majuto, “Tafadhali sana naomba unisaidie nimepata shida. Nyumba yangu ambapo nilikuwa nikiishi na
mtoto wangu mmoja na mjukuu wangu imeshika moto na kuteketea kabisa. Sina pakuishi wala chakula.
Ninakuomba unisaidie kwa lile utakalo weza.” Majuto alicheka kwa sauti kubwa, “ Ha ha ha, wewe bibi
kizee unatembelea magongo hata nikikusaidia wewe utaweza kunisaidia nini.” Hapo sauti ya Majuto
ilibadilika na aliongea kwa ukali sana, “Ondoka upesi sana hapa na usirudi tena! Nyie watu mnakuwa
hamna shukurani kabisa. Muda wote huu nimewasidia lakini mpaka leo mnaendelea tu kuja kwangu
kuomba misaada. Ondoka haraka na usirudi tena.” Masikini bibi kizee alianza kuondoka kwa
kunyong’onyea.
Ambacho Majuto alikuwa hajaona ni kuwa juu ya mti mkubwa uliokuwa kando yake yule ndege mkubwa
alikuwa amekaa na anaona yote yaliyokuwa yakitokea. Alitoa kelele kubwa kwa hasira “Ng’waaaa!”
Kisha ndege huyo aliruka na kutua mbele ya Majuto na kuongea. “Majuto, nimekupa kila ulichotaka na
kukuongezea mengine mengi. Sharti lilikuwa ni moja tu. Wape masikini na wasiojiweza nusu ya mapato
yako. Lakini hili umekuwa na tamaa na kusahau watu wengine.” Kwa maneno hayo ndege aligeuka na
alibakia hapo amesimama mchawi. Kumbe siku zote hizo Majuto hakujua kuwa yule ndege ndio mchawi.
Alikuwa amejigeuza ili aweze kumkumbusha majukumu yake kama tajiri. Lakini Majuto alizidiwa na
tamaa na kuamua kutojali watu wenye shida. “Mtaka vyote hupoteza vyote. Na wewe leo umepoteza
vyote. Hili liwe onyo kwako. ” Alisema mchawi.
Upepo mkali ulianza kuvuma kwa ngurumo mkubwa na vumbi lilitimka. Ardhi yote ilitetemeka na miti
ilitikisika. Majuto alifunga macho na kuziba masikio kwa uwoga. Baada ya muda mfupi upepo uliisha na
kila kitu kilitulia. Majuto alifungua macho yake taratibu na kuangalia huku na kule. Alidhani kuwa
amehamishwa kwenda sehemu nyingine. Nyumba yake na bustani na mali zake zote zilikuwa
zimetoweka. Mchawi naye pia alikuwa ametoweka. Kilikuwa kimebakia tu kibanda alichokuwa akiishi
zamani. Alianguka chini na kutoa kilio kikubwa.
Majuto aliamka tena na kutembea taratibu kwa kujivuta mpaka kwenye banda lake na kuchungulia
ndani. Aliona familia yake bado ilikuwepo na wote walikuwa wazima. Aliweza kusikia amani kidogo kuwa
hao bado walikuwa ni wazima. Majuto aliingia ndani ya banda na kutazama vizuri huku machozi bado
yanamtoka. Alishtushwa kuona kuwa bado nyavu alizokuwa amepewa na mchawi zilikuwa zimelala
kwenye mkeka.


“Hili litakuwa ni fundisho kwangu.” Alisema Majuto. Pamoja na masikitiko yake yote Majuto alikuwa
amejifunza kitu cha muhimu sana. Tamaa ya mali inakufanya usifikirie kuhusu shida za watu wengine.
Inabidi kumsaidia mtu mwenye shida pale unapoweza bila kubagua. Kuanzia siku hiyo Majuto alianza
kujenga maisha yake upya lakini alibaki kukumbukamaneno aliyokuwa akimkumbusha kila mara,
“Mtaka vyote, hupoteza vyote.” Na mpaka leo hii Majuto anaishi maisha mazuri sana kando mwa ziwa
na familia yake wakipendana na kusaidiana na watu wote wengine.

Majuto akiwa na familia yake wenye nyuso za furaha.

0 comments:

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Powered by Teknotaarifa