Wednesday, 1 June 2016

FAHAMU KUHUSU UFUGAJI KAA HAPA NCHINI NA CHANGAMOTO ZAKE.

                            
KAA ni jamii ya samaki ambao wanapatikana kwenye maji chumvi na maji baridi.
Wanaofugwa ni wale wanaopatikana zaidi kwenye maji chumvi. Mara nyingi hupatikana kwenye miamba ya mawe ambayo ipo majini. Mara nyingi vifaranga vya kaa vinapatikana kwenye miamba iliyoko kwenye mikoko ambapo wazazi wanataga mayai.
Mkurugenzi mkuu wa kampuni ya AQUES LTD Agnely Lishela anasema chakula chao kikubwa ni samaki na wadudu wadogo wadogo, kama minyoo inayopatikana baharini. Anaelezea ufugaji wa kaa hao unafanyika mara nyingi kwenye miti jamii ya mikoko ambako hujengwa vizimba ambavyo vina upana wa futi moja kwa futi moja.
“Kizimba kimoja kinaweza kuwa kimegawanyika katika vipande sita hadi nane, ambavyo vina uwezo wa kuchukua kaa wadogo sita mpaka nane,” anasema Lishela. Anasema kila chumba anakaa kaa moja mwenye uzito wa gramu 150, kaa huyo hukuzwa hadi afikie ukubwa wa kilo moja.
Anasema chakula kikubwa anacholishwa ni samaki wadogo. Kwa maelezo yake kaa hukuzwa kwa miezi mitatu ili wafikie kiwango cha kuuzwa kwa kilo moja. Akielezea matunzo yake anasema vizimba hivyo hujengwa kwenye maeneo ambayo maji hujaa na kutoka kwa sababu kaa wana uwezo wa kuhimili kwenye maji na nchi kavu.
Pia hufugwa kwenye eneo la maji masafi ili kuepukana na magonjwa ambayo yangeweza kuwaathiri. Jinsi ya kuwavua kaa hao anasema hufanyika pindi anapofikisha uzito wa gramu 800 hadi 1000. Na kwamba kwa soko la nje hupendelea sana kaa wafikishapo kilo moja.
“Kaa huweza kuvunwa muda wowote kwa lengo la biashara kwa soko la nje. Huvuliwa akiwa mzima na viungo vyake vyote viwe vimetimia na husafirishwa akiwa hai,” anasema. Anasema kwa soko la ndani kaa huweza kuuzwa akiwa chini ya gramu 800 na walaji wakubwa ni hoteli za kitalii. “Kwa wale ambao huonekana wamekufa hupelekwa sokoni huliwa na wenyeji wa maeneo hayo,” anasema.
Akielezea jinsi ya kuwasafirisha Lishela anasema kaa hao husafirishwa wakiwa hai kutoka kwenye shamba hadi kwenye masoko kwa soko la ndani na nje. Anasema uandaaji wake kwa wenyeji kaa huoshwa na kuuawa halafu huchemshwa.
“Wenyeji huwachukua kaa walio hai na kuwakata miguu kisha huwachemsha hivyo hivyo. Lakini kwa wale wanaosafirishwa huchemshwa hivyo hivyo bila kukatwa miguu wakiwa hai,” anasema. Akielezea changamoto zake anasema ugumu wa upatikanaji wa mbegu za kaa kwa kuwa wafugaji wengi wanategemea mbegu yake kutoka kwenye vyanzo vya asili.
“Hakuna kituo cha kuzalisha kaa nchini”. Anasema kwa kaa wanaofugwa huwa kuna wezi wengi wanaozunguka katika eneo husika. Pia maeneo ya ufugaji wa kaa hao yanakuwa ya wazi kila mtu anaweza kufanya shughuli zake.
Katika eneo hilo la ufugaji wa kaa kuna uhuru wa watu kuingia hivyo udhibiti wake unakuwa ni mgumu. Vile vile changamoto nyingine ni kwamba wafugaji wengi wa kaa ni wale wadogo wadogo hawana mitaji wala mbinu za kisasa za ufugaji hivyo inakuwa vigumu kutengeneza mazingira mazuri ya biashara.


0 comments:

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Powered by Teknotaarifa