Tuesday, 19 July 2016

FAHAMU KIUNDANI KABISA KUHUSU SAMAKI AINA YA KASA NA FAIDA ZAKE.

 NI samaki wa aina yake anayeishi katika kina kirefu cha maji ya bahari. Ana urefu wa sentimeta 170 na kilogramu 60. Ana mkia wenye ‘mapambo’. Una rangi ya bluu na madoadoa meupe.
Uvumbuzi wake unatajwa kuwa miongoni mwa uvumbuzi wa wanyama wenye kustaajabisha zaidi. Imezoeleka, samaki hutaga mayai kwa ajili ya kuzalisha vifaranga. Lakini kwa samaki huyu, huzaa. Naye si mwingine, bali ni samaki aina ya silikanti. Kwa lugha ya kigeni anajulikana Coelacanth.
Inaelezwa kwamba, mayai ya samaki huyu wa kike hayaanguliwi ndani ya maji. Badala yake, silikanti hutaga mayai mwilini na kuyaangua humohumo au mara tu yanapotoka mwilini huwa ni samaki.
Samaki huyu anapatikana hapa nchini. Huyu ni miongoni mwa vivutio vya utalii vinavyopatikana nchini ndani ya bahari ya Hindi kutoka Tanga hadi Mtwara.
Meneja wa Taasisi ya Hifadhi za Bahari na maeneo tengefu, Dk Milali Machumu anasema eneo ambalo anapatikana samaki huyo na ambalo limehifadhiwa kwa ajili ya utalii, limepewa jina la ‘Tanga Silikanti’. “Limeitwa Tanga silikanti kutokana na kuonekana kwa samaki huyo,” anasema Machumu.
Kiumbe huyu ni sehemu ya viumbe na vitu vingine vilivyoko baharini vinavyovutia watalii wengi hususani kutoka nje ya nchi. Kwa mfano, Dk Machumu anataja samaki mwingine mkubwa duniani, aitwaye walshake, kuwa anapatikana katika kisiwa cha Mafia.
Anamwelezea samaki huyu kuwa ni mkubwa, mpole ambaye watalii hupenda kuogelea naye. Lakini pia anataja samaki aina ya kasa ambaye pia hupatikana kwenye maeneo tengefu, kuwa ni kivutio kingine cha utalii nchini. Kwa mujibu wa Dk Machumu, kasa waliopo Mafia na Rufiji mkoani Pwani, wametambuliwa kimataifa kwa uwapo wao kwa wingi nchini.
Wakati kasa wapo wa aina tano, aina mbili ndio wapo kwa ajili ya kuzaliana na wengine hupita. Ikiachwa samaki hao wa aina mbalimbali, pia yako matumbawe, ndege wa kuvutia aina ya iron, na bustani za bahari, ambazo meneja huyo wa taasisi ya hifadhi za bahari na maeneo tengefu anasisitiza kuwa ni vivutio vikubwa vya utalii.
Wakati watu wengi huchukulia bahari kama sehemu ya kuvuna rasilimali, hususani kuvua samaki, Dk Machumu anasisitiza umma wa Watanzania kutambua kwamba pia ni eneo lingine la kitalii linalopaswa kutiliwa mkazo.
Anasema Tanzania ina vivutio mbalimbali ndani ya bahari ambavyo watalii wengi wanakuja kuvitazama na kusaidia kuongeza pato la taifa. Kwa mujibu wa Dk Machumu, awali watalii walikuwa wanakwenda Zanzibar lakini sasa wanatembelea katika visiwa vilivyopo Dar es Salaam, Tanga na Mafia. Utalii huo umenufaisha watanzania kwa kutoa ajira katika hoteli mbalimbali zinazojengwa kwenye visiwa hivyo na kujiongezea kipato chao.
Anasema watu wengi wamehamasika kupeleka huduma katika maeneo ya visiwa na kwamba asilimia 30 ya mapato wanayoyapata kutokana na utalii, asilimia 20 hupelekwa katika vijiji vinavyosaidia kutunza hifadhi na asilimia 10 katika wilaya.
‘’Rasilimali za bahari zipo nyingi na Tanzania imekuwa miongoni mwa nchi zilizobarikiwa kuwa na vivutio hivyo, kama vile matumbawe, bustani za bahari, mapango na samaki wa aina mbalimbali ambao sehemu nyingine hawapo kama vile samaki aina ya silikanti, kasa na ndege wa aina mbalimbali wanaopatikana baharini ambavyo huvutia watalii,’’ anasema Dk Machumu.
Anahamasisha watalii kuingia nchini kuwekeza katika visiwa hivyo ili kuongeza ajira na mapato ya taifa. Katika kuhakikisha hilo linawezekana, wameingia mkataba na wawekezaji mbalimbali wajenge hoteli zitakazosaidia utunzaji wa mazingira.
Watanzania wanahimizwa kujitokeza kwa wingi kutembelea visiwa hivyo. Mwito wa mtendaji huyo wa taasisi unatokana na kile anachosema, sasa watalii wengi kutoka nje ya nchi ndio hutembelea vivutio hivyo.
Dk Machumu ambaye taasisi yake ilianzishwa mwaka 1994 na iko chini ya Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi anasema kwa ajili ya kuhifadhi maeneo hayo, anataja maeneo tengefu yaliyopo nchini ni 15 ambako vivutio hivyo vinapatikana.
Anasema Dar es Salaam pekee ina maeneo tengefu saba yaliyoko Kaskazini na Kusini. Kwa upande wa Kaskazini, kipo Kisiwa cha Bongoyo, Mbudya na eneo tengefu la fungu la mchanga lijulikanalo kama Fungu Yasin na Pangamin.
Haya ni maeneo yaliyoanzishwa kabla ya taasisi hiyo haijaanza mwaka 1975 wakati Idara ya Uvuvi ilipokuwa inaanza. Maeneo hayo yalipitishwa kwa kutumia sheria ya Idara ya Uvuvi. Kusini vipo visiwa vya Finda, Kenda na Makatobe. Hivi vilianzishwa na kitengo cha Hifadhi za Bahari. Licha ya Dar es Salaam, maeneo mengine tengefu yako Mafia. Kisiwa hiki pia kina maeneo tengefu katika visiwa vya Shungimbili, Nyororo na Mbarakuni.
Kwa upande wa mkoani Tanga, kipo kisiwa cha Maziwe katika Wilaya ya Pangani. Miongoni mwa vivutio vilivyomo, ni kuwa kitovu cha mazalia ya kasa. Kasa huanguliwa kwenye fukwe za Ushongo na Kikokwe ndani ya kisiwa hicho. Maeneo mengine tengefu yanaanzia Tanga mjini hadi mpakani mwa Kenya, katika eneo la Horohoro.
Maeneo hayo ni pamoja na Mwewe, Kilui, Ulenge, Kwale pamoja na kisiwa cha Kilui kilichoko mpakani na nchi hiyo jirani. Kwa ujumla, anasema vipo visiwa vingi nchini ambavyo huhifadhiwa kwa ajili ya kujenga maeneo ya kitaliikutokana na rasilimali zilizopo.
‘’Hifadhi za bahari za Mafia zilianza mwaka 1995, Tanga silikanti ilianza mwaka 2009 na Guba Nazbay ambalo pia hupatikana gesi , lilianzishwa mwaka 2,000. Vipo visiwa vin gi nchini ambavyo vinatumika kama vivutio vya kitalii kwani wageni kutoka nje wanakuja kuviona,’’ anasema Dk Machumu. Anaelezea kitengo cha kusimamia hifadhi za bahari kinaruhusu wanajamii kuishi ndani ya hifadhi.
Anasema wanashirikisha wanajamii, kamati za mazingira za vijiji na wilaya katika kuhifadhi viumbe hai kuwa rahisi zaidi na kuondoa urasimu unaofanyika ndani ya bahari. Anatamani mafanikio wanayopata kwa kushirikiana na wanajamii ni pamoja na kuongezeka kwa akiba ya samaki baharini. Mafanikio mengine ni kuhifadhiwa kwa rasilimali na viumbe bahari walio katika hatari ya kutoweka kama vile mikoko, mwani. Hata hivyo, zipo changamoto zinazokabili vivutio hivyo vya utalii.
Mojawapo ni uvuvi haramu na uharibifu wa matumbawe ambayo hutumika kama mazalia na wakati huo huo chakula cha samaki. Serikali imelazimika kufanya mapitio ya sheria ya hifadhi za bahari na maeneo tengefu kutoa nafasi kwa maeneo ya maziwa, mito mikubwa na ardhi oevu, kuhifadhiwa kwa lengo la kupambana na uharibifu wa mazingira na uvuvi haramu. Dk Machumu anasema mapitio hayo ya sheria itasaidia kuongeza wigo wa kuhifadhi na maeneo ambayo hayakuwepo.
Anataja maeneo yaliyohifadhiwa ni jumla ya kilometa 2,000. “Maeneo yenye maji pekee yana kilometa 164,000 lakini tunayoyahifadhi ni kilometa 2,000 pekee.
Tunategemea marejeo haya ya sheria yatasaidia kutupa mwanya kuhifadhi maeneo ya maji baridi ili kupambana na uvuvi haramu,’’ anasema.
Changamoto nyingine ni ukosefu wa vyombo vya usafiri na maeneo ya kulala watalii kwenye maeneo ya utalii. Pia gharama kubwa za huduma za hoteli zinasababisha wananchi wa kawaida kutozimudu.
Pia mabadiliko ya tabia ya nchi yanayosababishwa na binadamu yanachangia baadhi ya visiwa kupotea. Wakati huo huo, umasikini kwa watu husababisha kufanya vitendo visivyo sahihi ikiwemo vya kuvua kwa kutumia mabomu.
Dk Machumu anatamani changamoto hizi zote ziondolewe hatimaye, viumbe hai na wasio hai wa bahari na maeneo tengefu, waendelee kuwa kivutio kwa watalii wa ndani na nje na mapato ya nchi yaongezeke..

0 comments:

Twitter Delicious Facebook Digg Stumbleupon Favorites More

 
Powered by Teknotaarifa